ALIYEISHI NA FISTULA KWA MIAKA 38 APATIWA MATIBABU, JUMLA YA WANAWAKE 16 WAFANYIWA UPASUAJI

Posted on: June 28th, 2024


Na SRRH

WANAWAKE 16 ambao wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la ugonjwa wa Fistula mkoani Shinyanga, wamefanyiwa upasuaji huku wengine nane (8) wakitarajiwa kufanyiwa leo Juni 28, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

Zoezi la upasuaji huo limefanyika bure katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kupitia Kambi ya Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake kutoka Hospital ya Rufaa Bungando Jijini Mwanza, Matibabu yaliyofadhiliwa na Shirika la Americares.

Mwakilishi kutoka Shirika hilo la Americares Dkt. Jonas Kagwisage, amesema wamekuwa wakitoa huduma hiyo kwa miaka 13 ya Matibabu bure ya Fistula kwa wanawake, kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wa wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando, na awamu hii wameweka kambi mkoani Shinyanga kutoa huduma hiyo.

Ameeleza katika Mkoa wa Shinyanga wameanza Kambi hiyo tangu Juni 23 ambayo itahitimishwa kesho Juni 29, huku akieleza kwamba hadi sasa wameshawafanyia Upasuaji wa Ugonjwa huo wa Fistula wanawake 16 na leo watawafanyia wengine Nane ambapo jumla watafikisha idadi ya wanawake 24.

“Huduma hii ya Matibabu ya Ugonjwa wa Fistula inatolewa bure, Shirika la Americares ndiyo tunagharamia kila kitu hadi chakula na nauli za kuwaleta hapa Hospitali, na tutawarudisha kwao,” amesema Kagwisage.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza Elieza Chibwe, amesema tatizo la Ugonjwa wa Fistula bado ni kubwa sana kwa wanawake ambalo husabishwa na uchungu pingamizi kwa mwanamke anapokuwa mjamzito, npia huchagiza kutokea kwa tundu ambalo linaunganisha njia ya uzazi na sehemu ya haja kubwa na ndogo ambapo hupelekea mwanamke kutokwa na kinyesi na haja ndogo muda wote.

“Ugonjwa wa Fistula ni ugonjwa wa aibu na matibabu ya Fistula ni Upasuaji tu, tunataka hadi kufikia 2030 tatizo la Fistula liishe kabisa”, amesema Dkt. Chibwe.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga Dkt. Luzila John, ameshukuru kwa utolewaji wa tiba hiyo, akieleza huduma ambayo pia imewajengea uwezo Madaktari wa Magonjwa wa wanawake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga na akibainisha watakuwa wakitoa huduma hiyo bila kuwapa wagonjwa Rufaa ya kwenda Bugando.

Naye Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Zamda Shabani, amelishukuru Shirika la Americares kwa kufadhili tiba hiyo, pamoja na Madaktari kutoka Bugando huku kutoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo ili waondokane na tatizo hilo.

Diwani wa Mwawaza, Mhe. Juma Nkwabi, ameiomba Serikali ipeleke pia Madaktari Bingwa wa kutoa huduma ya Fistula katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ili kurahisisha huduma ambayo itasaidia kutotegemea Madaktari wa Bugando.

Aidha, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Shinyanga, Bi. Halima Hamis, ambaye ndiye aliyeratibu zoezi hilo la Madaktari Bingwa, ametoa wito kwa wanawake wa Mkoa huo wapende kwenda katika vituo vya afya kwa ajili ya kujifungua, akieleza kuwa ni sehemu salama, sababu tatizo la Fistula huwakumba wajawazito ambao hujifungulia majumbani.

Mmoja wa wanawake ambaye amefanyiwa upasuaji, Bi. Terezia Mayunga kutoka Manispaa ya Kahama, amesema ameishi na tatizo la Fistula kwa miaka 38, lakini sasa amepatiwa Tiba na hali yake ni nzuri, huku mwingine akibainisha kwamba baada ya kupatwa na tatizo hilo, mume wake alimkimbia na sasa amepona.