DKT. LUZILA: MAGONWA YASIYOAMBUKIZA YANATIBIKA
Posted on: November 14th, 2023
INAELEZWA kuwa magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza ambayo ni pamoja na Shinikizo la damu, Saratani za aina zote, Kisukari, Figo, Mapafu na Magonjwa ya Moyo, yanatibika kwa kiwango kikubwa endapo tu matibabu yataanza mapema.
Hayo yamebainishwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Dkt. Luzila John, wakati akizungumza na Redio Faraja kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza, ambayo hufanyika kila mwaka wiki ya pili ya mwezi Novemba.
Dkt. Luzila amebainisha kuwa, endapo jamii itajenga utaratibu wa kwenda kupima magonjwa hayo mara kwa mara hata bila ya kuwa na dalili zozote, watalaamu wanaweza wakagundua mapema viashiria vyake na kuanza matibabu pamoja na kutoa ushauri juu ya kujikinga pia namna ya kuishi vizuri ili kudhibiti madhara makubwa ambayo yanaweza kutokea.
Amesema watu wengi wanapata madhara makubwa ya kiafya ikiwemo ulemavu wa kudumu na vifo, kutokana na kutojenga utaratibu wa kwenda kufanya uchunguzi wa afya zao, na wanafanya hivyo tu pale dalili zinapoanza kuonekana ambapo inakuwa vigumu kupona zaidi ya kupata matibabu tu ya kutuliza na kwamba, hatua hiyo inayafanya magonjwa hayo kusababisha vifo kwa zaidi ya asilimia 70 ikilinganishwa na magonjwa yale ya kuambukiza.
Dkt. Luzila amezitaja sababu zinazochangia watu kuungua magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza kuwa ni pamoja na mtindo wa maisha, hali ya Kibaiolojia (watu wanaotoka kwenye familia zenye historia ya kuugua magonjwa hayo) na umri.
Dkt. Luzila ameishauri jamii kujenga tabia ya kwenda Hospitali mara kwa mara kufanyiwa uchunguzi wa kiafya kuhusu magonjwa hayo na mengine, kubadili mtindo wa maisha kwa kufanya mazoezi, kufuata kanuni nzuri za ulaji, kupunguza uzito na kuepuka matumizi makubwa ya Pombe na tumbaku.
Katika kuadhimisha wiki ya magonjwa yasiyoambukiza, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga kuanzia Jumatatu ya Novemba 13 hadi Ijumaa Novemba 17, 2023, imekuwa ikitoa bure huduma za vipimo na ushauri kwa magonjwa yote yasiyokuwa ya kuambukiza, ambapo Dkt. Luzila amewaomba wananchi wote kutumia fursa hiyo kufika Hospitalini ili kufanyiwa uchunguzi.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza kwa mwaka huu inasema kuwa "IJUE HATARI YAKO, FAHAMU MAJIBU YAKO".