HOSPITALI YA RUFAA MKOA SHINYANGA YAFANYA SHEREHE KWA WATOTO NJITI

Posted on: December 8th, 2023


Na Shinyanga RHH

HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga kupitia Idara ya Watoto, leo Disemba 08, 2023 imefanya Sherehe Maalumu ya kuwapongeza Watoto Njiti ambayo Maadhimisho yake Kitaifa yalifanyika Novemba 17, 2023.

Katika sherehe hiyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali, Dkt. Luzila John ametoa pongezi kwa Wauguzi na Madaktari kwa kujitoa kuwahudumia watoto pamoja na Wazazi wao ambao walikaa wodini kwa miezi kadhaa.

Dkt. Luzila ametoa pongezi pia kwa kuandaliwa sherehe ya kuwajali watoto hao, huku akiwataka watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia miiko ya kazi pamoja na kuendelea kushirikiana ili kupuguza vifo kwa watoto njiti.

“Niwapongeze kwa kuandaa sherehe hii nzuri kwani inaonesha namna gani mnawajali watoto njiti, lakini vilevile nawaomba tuendelee kuonesha ushirikiano kuboresha huduma kwa watoto hawa ili waweze kuishi”, amesema Dkt. Luzila.

Kwa upande mwingine, Dkt. Luzila amewataka watumishi kujitahidi kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa pamoja na mrejesho wakati wa kutoa huduma, ili kuongeza uaminifu na kuwafanya wajisikie vizuri.

Amebainisha hilo akieleza lugha nzuri inamfanya mgonjwa ajione amefarijiwa pamoja na kumfanya avutiwe kurejea tena Hospitalini kuhudumiwa, vilevile akiipongeza serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma katika Kitengo cha Mama na Mtoto.

Aidha, katika kupunguza vifo vya Mama na Mtoto pamoja na watoto wanaozaliwa chini ya umri, Afisa Muuguzi Msaidizi Idara ya Watoto Wachanga (NICU), Neema Namgali, amesema Wauguzi na Madaktari wanao wajibu wa kutoa elimu kwa akina mama hususani dalili za hatari za ujauzito, kuhudhuria kliniki.

Bi. Nangali ameeleza kwa kawaida mtoto anapaswa kuzaliwa akiwa na kilo 2.5, akieleza ili kusaidia watoto wasiwe chini ya kilo hizo, ni vema wataalamu wa afya wakawajibika kuwakumbusha akina mama wajawazito yapi wanayopaswa kuzingatia kabla hawajafikia hatua ya kujifungua.