ANUDHA YATOA ELIMU YA VIFAA TIBA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA SHINYANGA

Posted on: September 25th, 2023


Na SRRH

KAMPUNI ya Anudha inayojihusisha na masuala ya Uingizaji na Usambazaji wa Vifaa Tiba nchini, Septemba 25, 2023 imetoa mafunzo ya matumizi ya Vifaa Tiba watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Mwezeshaji Marco James ambaye ni Muuguzi Bingwa wa Wagonjwa Mahututi na wa Dharura katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Bugando, ameeleza mafunzo yamelenga zaidi katika kuhakikisha matumizi sahihi ya vifaa tiba walivyosambaza katika Hospitali za Rufaa, yanafanyika kwa usahihi ili kuokoa maisha ya wagonjwa.

Mwezeshaji Marco James akitoa elimu ya matumizi ya Vifaa Tiba kwa watumishi wa Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

“Anudha wameona ni vema kuandaa mafunzo ambayo yatasaidia kukumbusha matumizi sahihi ya vifaa tiba wanavyogawa, ili kusaidia kutazama hali za kiafya kwa wagonjwa kwa ajili ya kufanya matibabu sahihi.

“Lakini pia tumekuja kufanya mafunzo haya ukizingatia kuna watumishi wapya walioajiriwa, hivyo tuliona ni vema tukaja kukumbushia ili kila mtumishi aweze kuvitendea haki vifaa hivi kiusahihi”, amesema.

Kwa upande wake Cyprian Mwagike ambaye ni Afisa Masoko wa Kampuni ya Anudha Limited, amesema Anudha wamekuwa na utamaduni wa kufanya mafunzo ya mara kwa mara kwa vifaa ambavyo wamekuwa wakivigawa Hospitalini ili kuboresha matumizi yanayotakiwa kwa ufasaha.

Mwagike ameeleza mbali na watumishi wa afya kutekeleza majukumu yao kwa kutumia vifaa tiba hivyo kwa usafaha, lakini pia kuvitunza vizuri ili viweze kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika.

“Tunatoa mafunzo ili kutoa usahihi wa matumizi kwa vifaa tiba tulivyogawa na huwa tunafuatilia kuona kama matumizi yanaenda namna inavyotakiwa, haitakuwa sawa kuona vifaa vinaharibika wakati Serikali imegharamika kununua vifaa hivi kwa gharama kubwa”, amesema Mwagike.

Mwezeshaji Cyprian Mwagike akitoa elimu ya matumizi ya Vifaa Tiba kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

Aidha, Mwagike ametoa wito kwa watumishi wote wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga hususani walipata mafunzo, kuwa Walimu wazuri kwa watumishi wengine ambao hawakupata mafunzo, na kwa waajiriwa wapyaa ili kuboresha matumizi sahihi ya vifaa tiba.

Mafunzo haya ambayo  yameanzia ukanda wa Hospitali za Rufaa Kanda ya Ziwa, yamelenga zaidi katika Vifaa Tiba kama ECG, Fluid Warmer na vingine ambavyo Anudha ilivigawa.