DKT. LUZILA AWATAKA WALINZI NA WAFANYA USAFI KUWAJALI WATEJA KWA KUZINGATIA MAADILI YA KAZI

Posted on: October 26th, 2023


Na SRRH

WAHUDUMU wanaohusika na shughuli za Ulinzi na Usafi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) wameaswa kufuata kanuni na maadili ya kazi ikiwemo kutumia lugha nzuri kwa wateja ambao ndiyo kipaumbele mama ili kuboresha huduma za afya Hospitalini.

Hayo yamesemwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Luzila John wakati akifungua Kikao cha Mafunzo maalumu kwa Walinzi na wafanya Usafi kilichofanyika leo Oktoba 26, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Hospitalini.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga, Luzila John, akizungumza na wahudumu wa Ulinzi na Usafi.

Dkt. Luzila amebainisha kuwa lugha nzuri kuanzia getini inasadia kumpa taswira chanya mteja (mgonjwa) anapoingia Hospitali kwa ajili ya kwenda kuhudumiwa, na inasaidia kumjenga katika hali ya imani pindi anapoenda kuhudumiwa.

“Matumizi ya lugha nzuri ni kitu cha msingi kwa wateja, tuwasikilize wateja wetu vizuri, tuwakarimu pia tuachane na lugha za kibabe.

“Kuna wakati mteja anaweza akawa hayuko vizuri na akakujibu vibaya, haimaanishi na wewe umjibu vibaya, badala yake angalia namna nzuri ya kuongea naye ili afurahie huduma zetu”, amesema Dkt. Luzila.

Wahudumu wa Ulinzi na Usafi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, wakisikiliza yanayowasilishwa kwenye kikao.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Luzila amewataka wahudumu hao kuishi kwa upendo ili kuboresha huduma Hospitalini, akieleza upendo unaleta matokea chanya na uwajibikaji mzuri kazini, huku akibainisha bila upendo, Mungu hawezi kubariki kazi za mikono yao.

Kwa upande wake Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali, Bi. Selina Mpemba, amesisitiza utekelezaji wa yale yote yaliyofundishwa kwenye kikao, ikiwemo matumizi ya lugha nzuri pamoja na kuepukana na masuala ya rushwa, kitu ambacho kinachangia kwa ukubwa kuchafua taswira ya taasisi.

Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Bi. Selina Mpemba akizungumza kwenye kikao.

"Nawaomba tujikite zaidi kwenye matumizi mazuri ya lugha, tuachane na rushwa ambayo inachafua Ofisi, kila mtu atambue wajibu wake ili kuiweka Taasisi kwenye hali ya ueledi", amesema Bi. Mpemba.