DKT. MAUFI: ASILIMIA 30-40 YA WANAWAKE SHINYANGA WANAKABILIWA NA TATIZO LA UGUMBA

Posted on: October 30th, 2023


Na SRRH

WANAWAKE Mkoani Shinyanga wameelezwa kukabiliwa na tatizo kubwa la ugumba kwa kukosa watoto, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoaji wa mimba holela, matumizi ya dawa za kuzuia mimba, maradhi ya uzazi na magonjwa ya zinaa.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akina Mama na Uzazi katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Augustino Maufi, amebainisha hayo wakati akizungumza na Gazeti la Nipashe, kujua hali ikoje ya tatizo la ugumba kwa wanawake mkoani Shinyanga.

Amesema tatizo la ugumba kwa wanawake katika Mkoa wa Shinyanga ni kubwa, na asilimia 40 wanakabiliwa na tatizo la Mirija ya Uzazi kuziba na kusababisha kutopata watoto.

“Tatizo la ugumba kwa wanawake katika Mkoa wa Shinyanga ni kubwa, ukiangalia kwenye Kliniki ya Magonjwa ya Akina mama ambayo hufanyika mara mbili kwa wiki, Jumatatu na Alhamisi asilimia 30 hadi 40 shida yao kubwa ni matatizo ya ugumba,” amesema Dkt. Maufi.

Aidha, Maufi ametaja baadhi ya sababu kubwa ambazo zimekuwa zikisababisha wanawake kukabiliwa na tatizo la ugumba, kuwa ni utoaji mimba hovyo, matumizi holela ya madawa ya kuzuia mimba ikiwamo P2, maradhi katika mfumo wa uzazi, magonjwa ya zinaa kikiwemo kisonono na kusababisha mirija ya uzazi kuziba.

Vilevile amebainisha kuwa tatizo la ugumba halipo kwa akina Mama pekee, bali hata kwa Wanaume ambao nao wanakabiliwa na tatizo hilo kwa mbegu zao kushindwa kutunga ujauzito.

Dkt, Maufi ameeleza tatizo la ugumba linatibika, na endapo wahusika watawahi kupata tiba na kuzingatia ushauri wa Daktari, huku akiwataka akina mama wanaopatiwa huduma hiyo, kutosikiliza ushauri wa watu wasio wataalamu wanaowataka kusitisisha dozi husika.

Katika kuhakikisha Afya ya Mama na Mtoto inakuwa salama, Dkt. Maufi ametoa wito kutoa wito kwa wanandoa ambao wanakabiliwa na tatizo la kukosa watoto, wahudhurie wote kwenye huduma za afya hususani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga kwa huduma ya vipimo na matibabu.