MAFUNZO YA TIBA MTANDAO YATOLEWA HOSPITALI YA RUFAA MKOA SHINYANGA

Posted on: October 24th, 2023


Na SRRH

WATAALAMU kutoka Wizara ya Afya pamoja na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) wametoa mafunzo ya Tiba Mtandao (Telemedicine) kwa Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga kwa lengo la kuwajengea uwezo.

Dkt. Liggyle Vumilia ambaye kutoka Wizara ya Afya Idara ya Tiba, amesema mafunzo hayo yatasaidia kuhudumia wananchi walio mbali na Hospitali bila kusafiri umbali mrefu.

“Lengo kubwa la kuja katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga ni kuhakikisha inaunganishwa na Huduma za Tiba Mtandao (Telemedicine) ili kusaidia kumhudumia mwananchi aliye pembezoni na mji ama mbali bila kusafiri umbali mrefu”, amesema Dkt. Vumilia.

“Mwananchi anaweza akapigwa picha ya CT-Scan, X-Ray (ambazo zote zimefungwa hapa), picha hiyo inaweza ikatoka hapa na kwenda Hospitali nyingine kisha kusomwa na Mtaalamu Bingwa, na majibu yatarudishwa hapahapa Shinyanga na mgonjwa atafanyiwa maamuzi ya Kidaktari kisha kutibiwa akiwa hapahapa Shinyanga”, amesema.

Kwa upande mwingine Dkt. Vumilia amesisitiza Hospitali zijikite zaidi kuwekeza kwenye matumizi ya mfumo wa Tiba Mtandao ili kusaidia zaidi huduma zifanyike vizuri, pamoja na kusaidia kupunguza gharama za wagonjwa kusafiri umbali mrefu.