HUDUMA YA CT SCAN HOSPITALI YA RUFAA SHINYANGA YAPUNGUZA GHARAMA ZA WAGONJWA
Posted on: July 20th, 2023Na SRRH
HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga imefanikiwa kunufaisha zaidi ya wagonjwa 150 kutokana na uwepo wa huduma ya CT SCAN ambayo imeanza rasmi kufanyika hivi karibuni.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Dkt. Luzila John, amesema uwepo wa huduma hiyo umepunguza gharama za wagonjwa kusafiri umbali mrefu kwenda Hospitali zingine kwa ajili ya kupata huduma.
“Huduma imepunguza vifo na gharama za safari kwenda Hospitali zingine kwa ajili ya vipimo, kwa sasa tunahudumia wagonjwa kutoka Wilaya za Mikoa mikoa ya jirani ikiwemo Tabora, Geita pamoja na Simiyu ukizingatia mpaka sasa tumepokea zaidi ya wagonjwa 150”, amesema Dkt. Luzila.
Kutokana na uwepo wa huduma hiyo, wagonjwa mbalimbali wametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kusaidia na kuboresha sekta ya Afya, hususani ujio wa huduma ya CT SCAn katika Hospitali ya Rufaa Shinyanga.
Aidha, wameeleza uwepo wa huduma hiyo umesaidia kupunguza gharama za kwenda Hospitali ya Rufaa Mkoa Mwanza (Sekou Toure) ambayo walizoea kwenda kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za afya.