MADAKTARI TARAJALI, WAFAMASIA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA RUSHWA PIA KUWAJIBIKA KWA UADILIFU

Posted on: October 18th, 2024


Na George Mganga, Shinyanga RRH

MADAKTARI Tarajali na Wafamasia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, wametakiwa kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo ya afya, ikiwemo kuepuka rushwa pindi wakiwa wanaendelea na mafunzo ya kazi.

Akizungumza katika kikao maalumu alichoitisha leo Oktoba 18, 2024, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga, Luzila John, ameeleza hayo kwa msisitizo, lengo ikiwa ni kuhakikisha mteja anahudumiwa kwa kufuata miongozo na usawa wa huduma.

Dkt. Luzila amewaeleza Madaktari hao tarajali na wafamasia kuhakikisha wanajiepusha na suala la rushwa, huku akitoa onyo kwa yeyote atakayebainika kujihusisha atakuchukuliwa hatua kwa haraka zaidi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga, Luzila John, akizungumza na Madaktari Tarajali pamoja na Wafamasia.

“Kila mtu achukie rushwa, unaweza mtoza mgonjwa rushwa lakini ukaja kupatwa na changamoto nyingine ya kimaisha hapo baadaye kwa maana Mungu anajua namna ya kulipiza ubaya kwa namna nyingine.

“Rushwa ni adui wa haki, naomba tuachane na hii tabia ambayo ni kinyume na miongozo ya kazi. Hata kama si waajiriwa, mkiwa mafunzoni mnapaswa kufuata miongozo ya utumishi wa umma”, ameeleza.

Aidha, Dkt. Luzila amekumbushia utoaji wa huduma kwa usawa bila kujali hadhi na muonekano wa mgonjwa kuwa ni jambo muhimu zaidi kuzingatiwa.

Ameeleza kila anayefika hospitali kuhudumiwa ana haki ya kupewa kipaumbele na si kuangalia aina ya mtu, jambo ambalo halina ustawi mzuri kwa afya ya mgonjwa.

“Kila anayefika kuhudumiwa ahudumiwe kwa haki na usawa, kuna baadhi wanatoa huduma kwa kuangalia hadhi ama muonekano wa mtu, hiyo haitakiwi, mtibu mtu bila kumbagua,” amesema Dkt. Luzila.

Kwa upande mwingine Luzila amegusia pia kwa kuwataka madaktari na wafamasia hao kuwa na matumizi mazuri ya lugha, hususani kwenye utoaji wa taarifa ikiwemo mrejesho kwa wagonjwa, amesema ni muhimu zaidi kwani unamsaidia mgonjwa kujua maendeleo yake pindi anapoendelea kupata matibabu.