MAFUNZO YA KITITA CHA UZAZI SALAMA YAANZA KUTOLEWA
Posted on: May 6th, 2024
Na George Mganga, SRRH
KATIKA kuboresha na kuhakikisha watumishi wa Sekta ya Afya hususani kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa wanajengewa uwezo wa kutoa huduma kwa ubora unaotakiwa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH), leo Mei 06, 2024 imeanza kupata mafunzo ya Kitita cha Uzazi Salama (SBBC).
Mafunzo hayo yameanza yakiwa na lengo mama la kuboresha huduma ya mama na mtoto wakati wa uzazi na baada ya kujifungua, dhamira ikiwa ni kupunguza vifo vinavyojitokeza.
Wataalamu John Tuwaha (Mkufunzi wa SBBC kutoka Kitita cha Uzazi Salama Tabora), Savera Martin (Muuguzi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Mwanza) na Ndinisyu Daniel ambaye ni Daktari wa Magonjwa ya Akina Mama na Uzazi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Geita ndiyo wawezeshaji wa mafunzo hayo.
Teddy Mtani ambaye ni Mratibu wa zoezi hilo na Afisa Muuguzi Msaidizi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, amesema mafunzo yatafanyika kwa wiki moja kuanzia leo, huku akieleza yanalenga zaidi Idara za Wazazi, Watoto wachanga pamoja na Idara ya Upasuaji.
Kitita cha Uzazi Salama ni mchanganyiko wa vifaa vya kutolea mafunzo pamoja na huduma, vinavyoongozwa na takwimu ili kuwezesha uzazi salama kwa mama na mtoto, wakati na baada ya kujifungua.