MAFUNZO YA KITITA CHA UZAZI SALAMA YATOLEWA SRRH

Posted on: January 31st, 2024

Na SRRH

KATIKA kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa katika Sekta ya Afya, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (SRRH) kupitia Idara ya akina Mama na Uzazi, leo Januari 31, 2024 imetoa mafunzo kuhusiana na Kitita cha Uzazi Salama.

Experantia Misalaba ambaye ni Afisa Muuguzi Msaidizi kutoka idara hiyo, amebainisha mafunzo hayo ni muhimu huku akiwataka watumishi kuhakikisha wanafanya mazoezi kwa ajili kupata uzoefu utakaotumika kuwasaidia wengine kwa dhamira ya kupunguza vifo vya mama na mtoto.

“Mafunzo haya dhamira yake kubwa ni kupunguza vifo vya mama na mtoto, tumeamua kuyatoa kwa lengo la kukumbushana na kuwawezesha wengine ili kukuza wigo wa uelewa na uzoefu ili kuboresha huduma”, amesema.

Akitoa somo kuhusiana na matumizi ya MOYO ambacho ni kifaa maalumu cha kisasa kinachotumika kupima mapigo ya moyo kwa mtoto, Misalaba ameeleza umuhimu wake kuwa kinasaidia kuboresha huduma ya mama na mtoto.

Kitita cha Uzazi Salama ni mchanganyiko wa vifaa vya kutolea mafunzo pamoja na huduma, vinavyoongozwa na takwimu ili kuwezesha uzazi salama kwa mama wakati na baada ya kujifungua.