MAFUNZO YA UTUNZAJI TAKA YATOLEWA, WALIOFANYA VIZURI WAKABIDHIWA ZAWADI

Posted on: March 27th, 2024


Na SRRH

KITENGO cha Ubora wa Huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga leo Machi 27, 2024 kimetoa mafunzo kuhusiana na utenganishaji taka pia aina za taka katika maeneo mbalimbali ya Hospitali.

Akitoa mafunzo hayo, Mratibu wa Kitengo hicho ambaye pia ni Afisa Muuguzi Msaidizi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Nyachiro Mujaya, ameeleza dhamira ya kutoa mafunzo hayo ni baada ya kuona changamoto kadhaa za utenganishaji taka katika maeneo mbalimbali ya Hospitali.

“Kama kitengo cha kuratibu ubora wa huduma tumeona tutoe mafunzo haya kwa lengo la kukumbushana namna nzuri ya kuhifadhi taka kwenye vitunza taka (dustbin) ili kuepukana na changamoto za kiafya.

Mratibu wa Kitengo cha Ubora katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Bi. Nyachiro Mujaya

akitoa mafunzo kuhusiana na utunzaji taka kwa watumishi.

“Zoezi hili limefanyika baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Hospitali na kujionea changamoto baadhi ambazo zimetufanya tukumbushie aina za taka zinazozalishwa Hospitalini na namna ya kuzihifadhi mahala sahihi, ikiwemo matumizi ya rangi katika vitunza taka”, amesema Mujaya.

Kwa upande mwingine, katika kuhamasisha utoaji bora wa huduma na kwa viwango stahiki, kitengo hicho kilitoa zawadi kwa kwa baadhi ya idara na vitengo ambavyo vimefanya vizuri katika robo ya kwanza ya mwezi Julai hadi Septemba, 2023.

Waliopata zawadi hizo ikiwemo ngao, vyeti na kombe kwa robo ya kwanza ni CTC, Maabara, Utawala, Huduma ya Wagonjwa wa nje , Wagonjwa wa dharura na Wodi ya Watoto, na katika Robo ya Pili walipata zawadi ni NICU na Maabara.

Kufuatia kutolewa kwa zawadi hizo, Bi. Mujaya amewaomba ambao hawajafanya vizuri kuendelea kuonesha za uwajibikaji mzuri wa kazi kwa lengo na maslahi mapana ya kuboresha huduma za Hospitali huku akiushukuru uongozi kwa mchango na ushirikiano mzuri wanaounesha katika kutekeleza majukumu yanayostawisha maendeleo ya Hospitali.