MHE. SANTIEL AKABIDHI MITUNGI YA ORYX GAS 200 KWA WAUGUZI KUTOKA DORIS MOLLEL FOUNDATION
Posted on: July 9th, 2024
Na George Mganga, SRRH
MBUNGE wa Viti Maalum katika Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Santiel Erick Kirumba, amewaomba wauguzi wa Mkoa Shinyanga kutumia nishati safi ya kupikia, badala ya kuni ambazo huzalisha moshi wenye madhara kiafya, pia kuharibu mazingira.
Hayo ameyasema leo Julai 09, 2024 wakati akikabidhi jumla ya mitungi 200 kwa watumishi wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Hospitali ya Manispaa Shinyanga, Kituo cha Afya Kambarage, Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga na Kolandoto, iliyotolewa na wadau Doris Mollel Foundation pamoja na Kampuni ya uzalishaji gesi (Oryx Gas).
Mhe. Santiel ameeleza matumizi ya kuni yamekuwa sababu kubwa ya uharibifu wa mazingira, lakini vilevile huhatarisha afya haswa ya mama na mtoto tumboni, sababu si salama, huku akisisitiza kuwepo kwa matumizi mazuri ya gesi ambayo itasaidia kulinda usalama wa afya kwa mama mjamzito.
“Niwaombe wauguzi, mmekuwa mkipokea akina mama wengi katika maeneo yenu ya kazi ambao wanaelekea kujifungua, tutumie nishati safi ya kupikia ili kulinda maisha ya mama na mtoto.
“Tuachane kabisa na matumizi ya kuni ambayo huhatarisha afya ya mama mjamzito, licha ya hivyo kuni zinachochea moshi ambao una madhara kiafya, lakini vilevile ukataji wa miti unasababisha jangwa.
“Hii mitungi mliyopata mkaitumie vizuri na mkawe mabalozi wazuri kuhamasisha wengine wajikite na hii nishati safi ya kupikia ambayo hata Mhe. Rais, Mama Samia Suluhu Hassan amekuwa msitari wa mbele katika kuhakikisha watanzania wanatoka kwenye matumizi ya kuni hadi kwenye nishati safi ya kupikia”, amesema Mhe. Santiel.
Kwa upande wake Mratibu wa zoezi hilo kutoka Doris Mollel Foundation, Bi. Dorice Laurent, ametoa shukrani kwa kampuni ya Oryx iliyosaidia kupatikana kwa mitungi 200 ambayo itasawadia akina mama wajawazito katika shughuli mbalimbali za mapishi.
Bi. Laurent ameongeza kuwa, lengo lao kama Foundation ni kuhakikisha wanaendelea kugawa mitungi hiyo nchi nzima ili kuokoa maisha ya mama na mtoto, ambao wanakuwa kwenye hatari kubwa ya kupatwa na changamoto ya kiafya, pindi wanapotumia nishati isiyo salama katika shughuli za mapishi.
Aidha, Muuguzi wa Mfawidhi katika Mkoa wa Shinyanga, Bi, Frola Kajumulla, amewashukuru Oryx Gas na Doris Mollel kwa kugawa mitungi hiyo, akiamini itasaidia kuwa sehemu ya motisha kwa wengine, kutumia nishati safi ya kupikia.
Halikadhalika, Bi. Kajumulla ameishauri jamii kwa ujumla kuepukana na matumizi ya kuni ambayo kiafya si salama, kujikita kwenye nisharti safi ya kupikia ambayo ndiyo njia pekee itasaidia kutunza mazingira yanayomzunguka binadamu.