PROF. NAGU ASISITIZA UTOAJI WA ELIMU YA UPIMAJI WA AFYA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI
Posted on: January 23rd, 2024
Na SRRH
MGANGA Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Joseph Nagu amewataka watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga kutokaa zaidi ndani badala yake kwenda nje ya Hospitali ili kutoa elimu kuhusiana na Upimaji wa Afya.
Hayo ameyaeleza leo Januari 23, 2024 alipotembelea Hospitalini kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa utoaji huduma na miundombinu, kufuatia na uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu katika baadhi ya mikoa nchini ikiwemo Shinyanga.
Prof. Nagu ametoa msisitizo huo kwenda maeneo ya watu pamoja na kutumia zaidi vyombo vya habari ili kutoa elimu ambayo itawasaidia wananchi kuishi kwa kufuata miongozi ya afya.
“Tutumie vyombo vya habari vya hapa Shinyanga na nje ili tuwape elimu wananchi hususani kuhusiana na magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza haswa namna ya kupunguza visababishi kama kufanya mazoezi.
“Tukumbushie matumizi zaidi ya Sukari na Chumvi pia uvutaji wa Sigara na unywaji wa Pombe kuwa si salama kwa afya ya binadamu, tusikae ndani tukajisahau na nashauri kila mgonjwa anapokuja vema akapimwa Presha na Sukari ili kujua yupo kwenye hali ipi, vilevile na Figo,” amesema Prof. Nagu.
Katika hatua nyingine, Prof. Nagu amesisitiza kuwa matumizi ya lugha nzuri ndiyo faraja na matumaini makubwa kwa mgonjwa mara baada ya kuwasili Hospitali kupatiwa huduma.
Ameeleza mgonjwa anapokuja ni vizuri akatiwa faraja na si kukemewa, akibainisha Hospitali si sehemu ya kupiga kelele.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Mhe. Christina S. Mndeme akiwa ameambatana na Prof. Nagu katika Kata ya Idukilo, Wilaya ya Kishapu mkoani hapa kwa ajili ya kufuatilia visababishi vya mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu, amewataka wananchi kuacha kutumia maji ambayo si salama.
Mhe. Mndeme amezungumza hayo kwa wananchi wa Kata hiyo huku akitoa maelekezo kwa Watendaji wote wa Wilaya ya Kishapu kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo ambacho kitasaidia kuepusha baadhi ya wananchi kwenda kujisaidia kwenye vichaka, kitu ambacho huchochea kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.