RC MHITA AWAPOKEA MADAKTARI BINGWA WA JKCI KWA AJILI YA KUTOA HUDUMA ZA KIBINGWA KWA WANANCHI SHINYANGA

Posted on: August 18th, 2025


Na George Mganga, Shinyanga RRH

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, leo Agosti 18 amewapokea rasmi madaktari bingwa tisa (9) kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) waliofika mkoani kwa ajili ya kutoa huduma maalumu za afya kwa wananchi, hususan huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo na uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kwa kina mama yanayofanya na wataalam kutoka hospitali ya Aga Khan.

Mapokezi hayo yamefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na viongozi wa sekta ya afya, wawakilishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga pamoja na wataalamu wa JKCI ambao wameweka kambi ya siku tano hadi Agosti 22, 2025, pia Aga Khan.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mhita alisema kuwa ujio wa madaktari hao ni hatua muhimu na ya kihistoria kwa Mkoa wa Shinyanga kwani utawezesha wananchi kupata huduma za kibingwa karibu na makazi yao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu hadi Dar es Salaam.

“Tunawakaribisha kwa moyo wa shukrani madaktari wetu bingwa kutoka JKCI. Huduma hizi ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wetu, hususan wagonjwa wenye matatizo ya moyo pamoja na kina mama wanaohitaji uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi. Hii ni fursa adhimu ambayo inaleta matumaini mapya katika kulinda afya za wananchi wa Shinyanga,” amesema Mhita.

Ameongeza kuwa Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa imejipanga kuhakikisha mazingira rafiki ya utoaji huduma yanapatikana, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, alisema kuwa kambi hiyo ya siku tano ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu bora bila kujali eneo analoishi.

“Taasisi ya JKCI inatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na serikali za mikoa na hospitali za rufaa ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma stahiki. Kambi hii ni ishara ya dhamira ya serikali na taasisi yetu katika kuimarisha afya na ustawi wa jamii kupitia huduma jumuishi na za kibingwa,” amesema Dkt. Kisenge.

Wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani wanahimizwa kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizi ambazo zinatolewa na wataalamu bingwa wa kitaifa.