RC MNDEME AWATAKA WATUMISHI KUTUNZA VIFAA TIBA, AIPONGEZA HOSPITALI KUAJIRI KWA MIKATABA

Posted on: October 31st, 2023


Na SRRH

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Christina Solomoni Mndeme, leo Oktoba 31, 2023 amefanya ziara iliyolenga kufanya Ukaguzi wa Huduma zinazotolewa na Vifaa Tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Katika ziara hiyo, Mhe. Mndeme amepongeza juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazofanya ikiwemo kuiwezesha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga Vifaa Tiba vya kisasa ikiwemo CT SCAN na X-Ray.

Kufuatia uwepo wa vifaa hivyo ambapo awali wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani walilalizimika kwenda Hospitali ya Rufaa Kanda ya Bugando jijini Mwanza, Mhe. Mndeme amewataka watumishi kuhakikisha wanavilinda pia kuepusha mianya ya wizi wa dawa.

“Tusimamie vifaa tiba na dawa vizuri ili kuhakikisha huduma zinafanyika ipasavyo, tusiruhusu mianya ya wizi ifanyike sababu Rais Samia ameamua kuisaidia Hospitali hii, hivyo kuvitunza sisi wenyewe na yeyote atakayebainika kuhusika na wizi, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake”, amesema Mhe. Mndeme.

Katika hatua nyingine, Mhe, ameipongeza Hospitali kwa kuajiri watumishi 98 wa kujitolea ambao ni wa mikataba kupitia mapato ya ndani, pamoja na kupeleka baadhi ya watumishi masomoni ili kujiongeza kielimu.

“Nawapongeza kwa kuajiri watumishi 98, ni hatua kubwa kwenu na hongereni pia kufanya maamuzi ya kwenda kusomesha watumishi ili kustawisha utoaji wa huduma katika Hospitali hii”, amesema.

Kwa upande mwingine, Mhe, Mndeme amesema serikali itapambana kuhakikisha barabara yenye urefu wa kilomita tatu (3) kutoka mjini hadi Hospitali, inajengwa kwa kiwango cha lami ili kupunguza adha ya usumbufu kwa wagonjwa.