RMO NDUNGILE: WATUMISHI ZINGATIENI MIIKO NA MAADILI YA KAZI, MSIWE WAJUAJI JALINI WATEJA

Posted on: November 2nd, 2023


Na SRRH

MADAKTARI, Wauguzi, Wakunga na Wafamasia Mkoani Shinyanga wameaswa kuzingatia Miiko na Maadili ya kazi katika utumishi wao Hospitalini ili kuboresha huduma za afya kwa kujali maslahi ya wagonjwa ambao ndiyo walengwa wakuu wanaopaswa kuhudumiwa.

Hayo yamesemwa leo Novemba 2, 2023 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Yudas Ndungile, wakati akifungua Kikao cha Kiutendaji kati ya Wauguzi na Wafamasia wa Mkoa wa Shinyanga na Maofisa kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

Dkt. Ndungile ameeleza kusikitishwa na baadhi ya watumishi katika Sekta ya Afya ambao wamekuwa wakikiuka miiko ya kazi, kwa kuwataka waifuate na kuizingatia ili kustawisha maendeleo ya afya hususani kwa wateja huku akiwataka kuacha ujuaji.

“Tuimarishe mawasiliano yetu na wateja, tuaje ujuaji ambao hauna maana sababu hali ya sasa si kama ya zamani. Unaweza ukawa unakiuka maadili kumbe mteja akakurekodi hata kukupiga picha bila wewe kujua kutokana na teknolojia ilivyo kwa kipindi hiki.

“Tusijione kuwa sisi ni wataalamu zaidi kuzidi wagonjwa, siku hizi ni wengi walioelimika, hivyo tuongeze umakini kwa kuwajali pia kutumia lugha nzuri ya mawasiliano, wafarijike ili waridhishwe na huduma zetu”, amesema Dkt. Ndungile.

Katika hatua nyingine Ndungile ametilia mkazo kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Christina Solomon Mndeme ya kuacha kuendekeza matumizi ya simu (kuchati) wakati wa kumhudumia mteja.

Amekumbushia kwa kueleza si busara sababu inaonesha dharau kwa mgonjwa, na badala yake akashauri kama mtumishi anataka kutumia simu, ni vema akamjulisha mteja wake kabla ya kuitumia.

Naye Afisa Maadili ambaye pia ni Mkunga Mbobezi kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), Bi. Mwajuma Mutabazi, ametilia mkazo kwa kuwataka watumishi kuzingatia majukumu yao kwa kuzingatia viapo vyao vya kazi.

Mutabazi ameeleza kufanya hivyo kutasaidia kutoa huduma nzuri kwa mteja sambamba na kufuata miiko na maadili ya kazi, ikiwa ni pamoja na kutumia lugha nzuri kwa mgonjwa na si kumjibu ilimradi.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Luzila John, Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Flora Kajumulo, Beatus Mpogoza kutoka Baraza la Wafamasia, Ayubu Lazaro ambaye ni Mwanasheria wa TNMC pamoja na Deogratius Mwailenge, Kaimu Mfamasia wa Mkoa wa Shinyanga.