WALINZI WAKUMBUSHWA KUTOA HUDUMA BORA KWA MTEJA

Posted on: April 16th, 2024


Na SRRH

KITENGO cha Uboreshaji Huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, leo Aprili 16, 2024 kimeitisha kikao na Walinzi kwa ajili ya kukumbushana majukumu yao katika eneo la Hospitali ikiwemo kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

Hayo ameyabainisha Mkuu wa Kitengo hicho, Bi. Nyachiro Mujaya, ambaye pia ni Afisa Muuguzi Msaidizi, kwa kusema lengo na nia ya kikao hicho ni kukumbushana majukumu chanya ambayo Walinzi wanapaswa kuyatimiza.

Bi. Mujaya ameeleza taswira nzuri ya taasisi husika hususani hospitali huanzia getini pindi mgonjwa anapowasili, hivyo ili kujenga imani na hospitali ni vizuri wagojwa wakapokelewa kwa lugha ya staha na ukarimu.

“Tumeitisha kikao hiki ili kukumbushana majukumu, taswira chanya ya hospitali huanzia getini mgonjwa anapoingia, mnapaswa kumkarimu mgonjwa na kumsaidia pale anapohitahi msaada wenu.

“Tuzingatie pia matumizi ya lugha, mgonjwa anaweza kuja akiwa kwenye hali mbaya pengine kupelekea kutamka maneno ambayo si mazuri, sisi kama watoa huduma hatupaswi kumjibu vibaya, tumjibu kwa upole na ukarimu kama miongozo inavyosema, tukienda hivyo tutaboresha huduma”, amesema Bi. Mujaya.

Kuitishwa kwa kikao hicho imekuwa ni desturi na utaratibu wa mara kwa mara kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, lengo ikiwa ni kukumbushana wajibu na majukumu kwa Walinzi, ambao pia ni watoa huduma Hospitalini.