WANANCHI WATAKIWA KUZINGATIA MATUMIZI LISHE BORA ILI KUEPUKANA NA KISUKARI
Posted on: September 27th, 2023
Na SRRH
WANANCHI wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani wametakiwa kuzingatia matumizi ya Lishe Bora ili kuepukana na Ugonjwa wa Kisukari ambao unaweza kuathiri karibu kila kiungo katika mwili.
Hayo yamesemwa leo Septemba 27, 2023 na Afisa Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Sherida Madanka wakati akizungumza na Watumishi wa Afya kwenye Kikao cha Mwendelezo wa Elimu ya Vipindi vya Afya (CME) Hospitalini, Mwawaza.
Sherida ameibainisha kuwa, kwa wasio na Kisukari ni vema wakazingatia ulaji mzuri wa vyakula ikiwemo mboga za majani, halikadhalika matunda ili kuiweka afya katika hali ya usalama.
“Ili kuepukana na ugonjwa wa Kisukari ni vizuri kuzingatia lishe nzuri ikiwemo ulaji wa mboga za majani na matunda ambazo zina virutubisho vizuri vinavyoimarisha kinga ya afya”, amesema Sherida.
Mbali na ulaji wa mboga pamoja na matunda, Sherida ameshauri pia kuepukana na matumizi ya pombe, uvutaji sigara, matumizi ya vinywaji vyenye sukari nyingi, vitu ambavyo kwa ujumla vinapelekea kupata Kisukari.
“Matumizi ya pombe, sigara, vinywaji vyenye sukari nyingi si vizuri kuvitumia sababu ndiyo sehemu ya chanzo cha ugonjwa huu, hivyo naomba tutumie kwa wastani na si mara kwa mara”, amesema.
Kwa upande mwingine, Sherida amekumbushia umuhimu wa kucheki afya mara kwa mara kuwa unasaidia kujua maendeleo ya afya, na akiwataka wagonjwa wenye kisukari kuzingatia matumizi ya lishe sahihi ili kuzuia makali ya ugonjwa huo, kwa kuiweka afya kwenye hali ya usalama zaidi.
Vilevile, Sherida ameeleza mazoezi ya mwili kama kukimbia, kuruka Kamba n ahata kutembea yanasaidia kupunguza makali ya ugonjwa kwa wenye kisukari na kinga ya kuupata ugonjwa huo kwa ambao hawana.
Ugonjwa wa kisukari unaweza kuathiri karibu kila kiungo katika mwili, ikiwa ni pamoja na:- Moyo na mishipa ya damu, Macho, Figo, Mishipa, Njia ya utumbo, Ufizi na Meno.