WANAWAKE WATAKIWA KUJITOKEZA KWA WINGI KUPIMA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI

Posted on: September 17th, 2023


Na SRRH

WANAWAKE mkoani Shinyanga na mikoa jirani wametakiwa kuwa na desturi ya kupima Saratani ya Mlango wa Kizazi mara kwa mara, ili kuepukana na changamoto ya ugonjwa huo.

Muuguzi Mariarose Bernard, kutoka Kitengo cha Upimaji wa Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa akina mama Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, amebainisha kuwa upimaji wa Saratani hiyo utasaidia wanawake kutambua hali zao kwa kuepukana na changamoto za kiafya.

“Nawaomba wakina wajitahidi kuja kupima saratani mara kwa mara ili kujua hali zao, na nawaomba wasiogope sababu itasaidia kulinda afya zao.

“Umbali wa Hospitali usiwe sababu ya kutokuja kwani afya ndiyo mtaji, naomba wajitokeze kwa wingi sababu huduma zinatolewa bure”, amesema Mariarose.

Aidha, Mariarose amewaomba wazazi kuwapeleka watoto walio chini ya miaka 14 katika Vituo vya Afya kwa ajili ya kupata Chanjo ya ugonjwa huo ili kuweka afya zao katika hali ya usalama zaidi.

Katika hatua nyingine, Mariarose ameshauri kuepukana na ngono zembe pamoja pia uvutaji wa sigara, akieleza ni vitu ambavyo vinapelekea kukumbana na Saratani hiyo ambayo inahatarisha afya ya mama.

“Nashauri ni vyema wanawake wakaachana na ngono zembe, uvutaji wa sigara pamoja na kupunguza kuwa na wapenzi wengi ili kuepuakana na chanzo cha kupata saratani hii ambayo inaweza kuhabribu mlango wa kizazi”, amesema.