WATUMISHI WA AFYA SHINYANGA WATAKIWA KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI

Posted on: November 8th, 2023


Na SRRH

WATUMISHI wa Afya katika Hospitali ya Manispaa Shinyanga na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga wametakiwa kutoa huduma bora kwa wananchi ili kuridhisha jitihada za Serikali ambayo imewezesha upatikaji wa miundombinu pamoja na vifaa tiba.

Hayo yamesemwa leo Novemba 8, 2023 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Yudas Ndungile wakati akifungua Mafunzo ya Utoaji wa Huduma za Dharura, ambayo yamewezeshwa na Wataalamu kutoka Wizara ya Afya, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Mwawaza.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Yudas Ndungile, akizungumza na Watumishi wa Afya 

waliohudhuria mafunzo katika Ukumbi wa Mikutano, Mwawaza.

Amebainisha kuwa kwa kueleza Serikali imewekeza katika kuboresha miundombinu ya afya, huku akieleza deni lipo kwa watumishi kuhakikisha wananchi wanafurahia huduma bora kwakuwa tayari serikali imeshafanya kazi yake ya kuboresha miundombinu.

“Haya mafunzo yanayotolewa hapa kwa ajili ya kujengeana uwezo yakatumike kutoa huduma bora kwa wananchi. Ni matarajio yangu baada ya kukamilika tukatoe huduma bora, walau tusitofautiane na Hospitali kubwa kama Muhimbili na Bugando.

“Naomba tutoe huduma bora na tuwe na mpango kazi tutakaouzingatia hususani katika kupunguza vifo ili wananchi wafurahie matunda ya serikali inayopambana kila siku kuhakikisha miundombinu ya afya inaenda vizuri”, amesema Dkt. Ndungile.

Aidha, kwa upande mwingine, Dkt. Ndungile amewaasa watumishi wote kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na taaluma za kazi, halikadhalika kufuata kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa umma, sanjari na kuepuka masuala ya rushwa ili kustawisha huduma bora za afya.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Luzila John, ametoa rai kwa watumishi wote waliopata mafunzo hayo, wayatumie vizuri pia waende kuwajengea uwezo watumishi wenzao.

Ameeleza kuwa ujuzi ambao umetolewa kwa wachache ukatumike pia kuwasadia wengine kwa lengo la kuongeza wigo mpana wa huduma nzuri kwa wananchi.