WAUGUZI SRRH WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI PIA KUEPUKANA NA RUSHWA

Posted on: October 12th, 2023


Na SRRH

WAUGUZI katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na miiko ya kazi ikiwemo kuepukana na masuala ya rushwa ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 12, 2023 na Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Selina Mpemba, katika kikao maalumu na Wauguzi, kilicholenga kukumbushana maadili na uwajibikaji kazini.

“Tufanye kazi kwa ueledi na ufasaha kwa kuwajali wateja wetu ili tutoe huduma bora, tuwajali kama ambavyo tunajijali sisi kwa kuwathamini kwa kufuata miiko ya kazi.

“Tuachane na desturi ya kuomba rushwa kwani ni kinyume na maadili, tuepukane na hilo suala kwani linatuchafua sisi kama taasisi na serikali kwa ujumla”, amesema Selina.

Kwa upande mwingine ikiwa ni siku chache zimepita za Wiki ya Huduma kwa Mteja, Selina amesisitiza kwa kuwaeleza Wauguzi kuwa ni wajibu wa kila mmoja kumjali mteja kwa kutumia lugha Rafiki.

Ameeleza mawasiliano mazuri ambayo Muuguzi hususani lugha, yanasaidia kuleta faraja na uaminifu kwa mgonjwa pindi anapokuja Hospitali kupata huduma.

“Tutumie lugha nzuri tunapowasiliana na mgonjwa ili kumtia faraja na ajisikie vizuri hata kabla hajapata matibabu, ni wajibu wetu kulitekeleza hilo na ukizingatia tumetoka katika Wiki ya Huduma kwa Mteja, hivyo ni vema tukiyatekeleza hayo kwa haki”, amesema.