WAZAZI WASHAURIWA KUWALEA WATOTO KATIKA MAADILI MEMA KUEPUSHA TATIZO LA AFYA YA AKILI

Posted on: October 20th, 2023


Na SRRH

USHAURI umetolewa kwa Wazazi na Walezi kuhakikisha wanawalea watoto katika maadili mema ili kuepukana na tatizo la Afya ya Akili linalopekelea kutokea kwa matukio ya kujinyonga ambayo yamekuwa yakitokea hivi karibuni hususani katika Mkoa wa Shinyanga.

Hayo yamebainishwa na Daktari wa Afya ya Akili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Asnath Msemwa wakati akifanyiwa mahojiano maalumu na Kituo cha Redio (Jambo FM) baada ya kuripoti matukio manne mfululizo ya watoto wa kujinyonga ndani ya miezi miwili.

Dkt. Asnath ameeleza, kutokana na uwepo wa matukio hayo wazazi na walezi wanapaswa kuwalea watoto katika maadili stahiki, sambamba na kuchukua hatua pindi wanapoona wanaanza kujitenga ama kuonesha viashiria vyovyote ambavyo si vya kawaida ikiwemo kuwapeleka Hospitali.

“Matukio ya watoto ama mtu mzima kujinyonga mara nyingi yanasababishwa na msongo wa mawazo ambayo huathiri mfumo wa ubongo, na hii inaweza ikawa inatokana na historia ya familia husika pengine huko nyuma ilikuwa na matukio ya aina hiyo.

“Mtu mwenye tabia ya kujitenga, kula sana ama kutokula, hasira na mengine ambayo si ya kawaida ni baadhi ya dalili za msongo wa mawazo. Kama mzazi, ukiona dalili hizo unapaswa uchukue hatua ya kumlea vizuri pia kumpeleka Hospitali.

Aidha, katika kutatua changamoto hiyo, Dkt. Asnath ameshauri wazazi na walezi kuwafuatilia kwa ukaribu zaidi watoto na si kukimbilia kuwaadhibu ama kuwachapa (kwa Walimu mashuleni). Badala yake wawape elimu na kuwashauri vizuri, pia kuwapeleka Hospitali ili kupata elimu ya kina juu ya Afya ya Akili.