WAZIRI UMMY AIPONGEZA HOSPITALI YA RUFAA SHINYANGA AAGIZA AJIRA ZA MIKATABA

Posted on: July 13th, 2023

Na SRRH

WAZIRI wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu ameipongeza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga kutokana na uwajjibikaji mzuri kwa watumishi pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Hayo ameyasema leo Julai 13, 2023 baada ya kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga kwa lengo la kufanya Ukaguzi wa huduma zinazotolewa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, Halmashauri, Vituo vya Afya pamoja na Zahanati nchini, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake akitokea Mkoani Simiyu.

“Nitoe pongeza za dhati kwenu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga kutokana na uwajibikaji mzuri wa utoaji huduma za Afya kwa wananchi, hakika nimeridhishwa na nafurahishwa kuona ni namna gani mnavyompa hamasa Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha fedha.

“Nawaomba endeleeni kuonesha jituhada nzuri zaidi kwa kuboresha mazingira mazuri ya kazi, pamoja na ubunifu wenu mzuri kazini. Tuwajali wananchi kwa kuwapa huduma kwa wakati, kuboresha upatikanaji wa vipimo pamoja na dawa”, amesema Waziri Ummy.

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu akikabidhi vifaa tiba.

Aidha, mbali na pongezi hizo, Waziri Ummy ameagiza Hospitali zote nchini (Rufaa na Halmashauri) kuajiri Wataalamu wa Afya kwa Mikataba ili kuongeza wigo na nguvu ya kutoa huduma bora na haraka kwa Watanzania.

“Naagiza Hospitali za Rufaa za Mkoa na Halmashauri zote nchini kuajiri Wataalam wa Afya wa Mikataba ili tuendelee kutoa huduma bora Kwa Watanzania na kwa haraka”, amesema.

Pia, Waziri Ummy amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshafanya jukumu lake la kutoa fedha katika Sekta ya Afya huku akibainisha kuwa ni jukumu la Wataalam wa Afya kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu akiangalia mashine ya CT-SCAN katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali Afya za Watanzania ametoa fedha za majengo, ametoa fedha za vifaa na vifaa tiba, fedha za dawa sasa ni jukumu letu sisi watendaji kutoa huduma bora kwa Watanzania.” ameeleza Waziri Ummy.

Licha ya kukagua kukagua utoaji wa huduma, waziri Ummy pia alipata nafasi ya kukabidhi vifaa tiba vya wodi ya watoto wachanga mahututi.

Mbali na Waziri Ummy, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Johari Samizi akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Christina Mndeme, amempongeza Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi ili kuboresha huduma za Afya mkoani humo, na kuahidi maelekezo ambayo ameyatoa Waziri watayatekeleza.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Mhe. Johari Samizi akizungumza kwenye ziara ya Waziri wa Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile, akisoma taarifa ya huduma za Afya mkoani humo, amesema upatikanaji wa huduma umeimarishwa pamoja na upatikaji wa dawa kwa asilimia 89.9.

Amebainisha licha ya huduma hizo kuboreshwa, lakini bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo ya Upungufu wa watumishi na Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga pamoja na Magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) pia hakuna Jengo la kuhifadhia maiti (Mochwari).


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile akizungumza kwenye ziara ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Luzila John akitoa taarifa ya Hospitali kwenye ziara ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu.


Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga wakimsikiliza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.